KUPIKA MAHARAGE
Chambua maharage yako vizuri, yaoshe
halafu weka kwenye sufuria safi, weka maji kiasi kisha yachemshe mpaka
yaive.
Yakishaiva ipua, chukua sufuria safi bandika
jikoni likishakauka maji mimina mafuta ya kula yaache yapate moto.
Baada ya hapo weka vitunguu maji ambavyo
umevikatakata vipande vidogovidogo, kaanga mpaka vibadilike rangi na kuwa vya
kahawia (brown), weka karoti ambazo umekata vipande vidogovidogo.
Vikishaiva weka maharage uliyochemsha na chumvi
kiasi, vikishachanganyikana weka tui la nazi subiri lichemke kwa dakika tano na
hapo mboga yako itakuwa tayari.
WALI WA ILIKI
Pepeta mchele wako vizuri ili kutoa uchafu.
Chukua sufuria safi, weka maji yanayotosha kupika
wali wako kisha yabandike jikoni huku ukiweka chumvi, mafuta ya kupikia na
iliki halafu funika.
Yaache yachemke, baada ya hapo weka mchele ambao
tayari umeshauosha kisha koroga huku ukiangalia
kama
chumvi imekolea.
Baada ya hapo funika subiri maji yakikaukia geuza
ili uive pande zote.
Funika kisha subiri kwa dakika kadhaa geuza tena
kwa mara ya pili ukiona maji yamekauka kabisa, hapo wali wako utakuwa tayari
kwa kula.